Jumla ya makanisa 700 yamefungwa, mengi yakiwa ni makanisa madogo madogo yaliyoanzishwa hivi karibuni.
Kulingana na bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi, makanisa yanatakiwa kufwata taratibu za ujenzi wenye miundo msingi stahiki na shahada ya elimu ya theolojia kwa wachungaji.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana aliyepo Kigali anasema makanisa yasiyopungua 700 na msikiti mmoja tayari yamefungwa kutokana na kile ambacho bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi imetaja kuwa kushindwa kutimiza kanuni za ujenzi.
Mwandishi wa BBC mjini Kigali anasema ukaguzi wa wakuu wa serikali za mitaa bado unaendelea kutathmini makanisa zaidi yasiyotimiza masharti na pengine kufungulia mengine ambayo yamo mbioni kutimiza matakwa ya serikali.
Rwanda inajadili sheria mpya ambayo itahusu mashirika yenye misingi ya imani na dini yanayoendeshwa na wahubiri kuwa wahubiri hao lazima wawe na shahada za elimu ya theolojia.

