Alhamisi, 29 Machi 2018

Miguna Miguna Mwanasiasa wa upinzani atimuliwa tena kutoka Kenya na kupelekwa Dubai



Mwanasiasa wa upinzani Kenya aliyeidhinisha kiapo cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi' Januari Miguna Miguna ametimuliwa tena kutoka nchini humo.

Mwanasiasa huyo ametimuliwa huku mzozo kuhusu uraia wake ukiendelea.

Bw Miguna ameandika kwenye Facebook kwamba ameamka na kujipata yuko Dubai na kwamba anahitaji matibabu.

Amesema anafahamu kwamba kuna mpango wa kumpeleka London lakini anataka kupanda ndege ya kurejea Nairobi pekee.

Mwanasiasa huyo amesema amesindikizwa na afisa wa idara ya ujasusi na kwamba amemuona daktari uwanja wa ndege.

Amesisitiza kwamba hatasafiri kwenda popote ila kurejea Nairobi.

Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.

Mawakili wa Bw Miguna wamethibitisha kwamba aliondolewa nchini humo kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates iliyokuwa inaelekea Dubai.

Bw Miguna alikuwa amezuiliwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) tangu alipowasili Jumatatu adhuhuri.

Mwanasiasa huyo alikuwa anajaribu kurejea kutoka Canada ambako alikuwa amepelekwa baada ya kufurushwa kutoka Kenya kwa lazima mwezi Februari.

Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga Jumatano alisema waziri wa usalama nchini humo, mkuu wa polisi na mkuu wa idara ya uhamiaji watakuwa wamekaidi maagizo ya mahakama iwapo wangekataa kumwachilia huru.

Alikuwa ametoa ilani kwa watatu hao kufika mahakamani baadaye Jumatano lakini baada yao kukosa kufika akawapata na hatia ya kukaidi agizo la mahakama.

Aliahidi kutoa adhabu dhidi yao leo asubuhi.

Maafisa wa Kenya mnamo 6 Febuari walikuwa wamemfukuza kutoka nchini humo kutokana na mchango wake wakati wa kuapishwa kwa Bw Odinga.

Walisema mwanasiasa huyo hana uraia wa Kenya lakini ana uraia wa Canada.

Idara ya uhamiaji ya Kenya imekariri kuwa Miguna alipoteza uraia wa Kenya mwaka 1998 alipopewa uraia wa Canada wakati ilipokuwa ni kinyume cha sheria kuwa na uraia wa nchi mbili nchini Kenya.


Kuzuiliwa kwa Bw Miguna kumejadiliwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii Kenya, baadhi wakiunga mkono hatua hiyo lakini wengine wakiwashutumu maafisa wa uwanja wa ndege na serikali.

Mmoja wa mawakili wa Bw Miguna, Nelson Havi, ni miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kufichua kwamba Bw Miguna alikuwa ametimuliwa tena nje ya nchi hiyo.



Bw Miguna alikamatwa na polisi kwa mchango wake katika kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa "Rais wa Wananchi", hafla iliyofanyika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi mnamo 30 Januari.

Bw Miguna, ambaye pia ni wakili, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo ya Bw Odinga.

Serikali ilikuwa imeeleza hatua hiyo ya kiongozi huyo wa upinzani kuwa uhaini wa hali ya juu.




Bw Odinga anadai kwamba alimshinda Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 8 Agosti ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kutokea kwa kasoro nyingi.

    Muungano wa upinzani Kenya unaelekea ukingoni?

    Serikali yamfurusha Miguna Miguna kutoka Kenya

Mahakama iliamuru uchaguzi mpya ufanyike lakini Bw Odinga akasusia uchaguzi huo mnamo 26 Oktoba na kutangaza kwamba hakumtambua Bw Kenyatta kama rais halali wa nchi hiyo.

Baadaye aliongoza hafla ya kuapishwa kwake mnamo tarehe 30 Januari.

Mapema mwezi huu, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta walikutana katika mkutano ambao haukuwa umetarajiwa na wakahutubia wananchi moja kwa moja kupitia vyombo vya habari.

Waliahidi maridhiano na pia wakaahidi kuwaunganisha tena Wakenya.

Bw Miguna mnamo Jumatano alikuwa ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumanne kwamba alikuwa anazuiliwa chooni uwanja wa ndege na kwamba alikuwa amezuiwa kuwaona mawakili wake na jamaa zake.

Jumamosi, 10 Machi 2018

Rais pekee mwanamke Afrika kujizulu kwa tuhuma za ubadhilifu


Rais wa Mauritian Ameenah Gurib-Fakim

Rais wa Mauritian Ameenah Gurib-Fakim amekubali kuachia madaraka baada ya kutuhumiwa kutumia kadi ya benki yenye thamani ya dola za kimarekani elfu kumi iliyotolewa na shirika la msaada katika matumizi yake binafsi.

Rais huyo ataachia madaraka yake baada ya madhimisho ya miaka hamsini wa uhuru wa ya taifa lake wiki ijayo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Reuters,rais huyo amekana kosa hilo na kudai kuwa alirudisha fedha zote.

Rais huyo aliyeingia madarakani mwaka 2015 alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa nchini Mauritius.ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kwenye madhimisho ya Marais wa Mauritus.

Waziri mkuu wa nchi hiyo Pravind Jugnauth amewaambia waandishi wa habari kuwa rais Ameenah ataachia wadhifa wake kama ilivyopanga na kuongeza kwa kusema kuwa kipaumbele cha taifa hilo ndio kilichozingatiwa ili taifa hilo liendele kuwa nchi ya mfano.

Hata hivyo gazeti moja nchini humo lilichapisha uthibitisho wa nakala ambazo rais huyo alifanyia manunuzi ya vitu vyake vya thamani nchini Uingereza.

Jumamosi, 3 Machi 2018

Swahili BBC Swahili Uongozaji Yaliyomo Rwanda yaanza kufungia makanisa 700 kwa kutotimiza masharti yaliyowekwa

 Serikali ya Rwanda imeanza kutekeleza uamuzi wa kufunga makanisa ambayo hayajatimiza kanuni za ujenzi na vigezo vingine vinavyotakiwa kwa wachungaji wa makanisa hayo.

Jumla ya makanisa 700 yamefungwa, mengi yakiwa ni makanisa madogo madogo yaliyoanzishwa hivi karibuni.

Kulingana na bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi, makanisa yanatakiwa kufwata taratibu za ujenzi wenye miundo msingi stahiki na shahada ya elimu ya theolojia kwa wachungaji.

Mwandishi wa BBC Yves Bucyana aliyepo Kigali anasema makanisa yasiyopungua 700 na msikiti mmoja tayari yamefungwa kutokana na kile ambacho bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi imetaja kuwa kushindwa kutimiza kanuni za ujenzi.

Baadhi ya makanisa yanaendeshea ibada zao kwenye mahema,huku makanisa mengi yakifanyia ibada zao kwenye nyumba za kibiashara kama baa na mighahawa; na makanisa mengi yana kelele za kupita kiasi ilhali yamejengwa katikati mwa makazi ya wananchi.

Mwandishi wa BBC mjini Kigali anasema ukaguzi wa wakuu wa serikali za mitaa bado unaendelea kutathmini makanisa zaidi yasiyotimiza masharti na pengine kufungulia mengine ambayo yamo mbioni kutimiza matakwa ya serikali.

Rwanda inajadili sheria mpya ambayo itahusu mashirika yenye misingi ya imani na dini yanayoendeshwa na wahubiri kuwa wahubiri hao lazima wawe na shahada za elimu ya theolojia.
Wakosoaji wanaona kwamba hii ni sheria inayolenga kudhibiti makanisa wakati wengine wanaona kwamba ni sheria yenye lengo la kunyoosha makanisa ambayo siku hizi yamezongwa na migogoro ya ndani.

Mgonjwa apasuliwa ubongo kimakosa hospitali ya taifa ya Kenyatta(Kenya) , mkuu wa hospitali apewa likizo ya lazima


Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta nchini Kenya ametumwa kwenye likizo ya lazima baada ya mgonjwa ambaye hakufaa kufanyiwa upasuaji wa ubongo kufanyiwa upasuaji huo katika hospitali hiyo.

Hatua ya kumtuma Lilly Koros kwenye likizo ya lazima imetangazwa na Waziri wa afya Sicily Kariuki ambaye amesema hatua hiyo inakusudiwa "kupisha uchunguzi".

Kisa hicho ambacho kimewashangaza wengi kilitokea katika hospitali hiyo wiki iliyopita na leo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa maafisa wa matibabu ambao walihusika kueleza ilikuwaje hadi kosa hilo likatokea.

Taarifa ya Bi Koros iliyotolewa Alhamisi ilisema maafisa wanne wa matibabu walikuwa wamesimamishwa kazi, akiwemo msimamisi wa sajili ya watu wanaofanyiwa upasuaji wa ubongo.

Wengine ni mwuguzi aliyekuwa akisimamia wadi, mwuguzi wa kuwapokea wagonjwa kwenye chumba cha kufanyiwa upasuaji na afisa wa kuwatia ganzi wagonjwa.

Bi Koros alisema kupitia taarifa kwamba kosa hilo lilitokea pale mkanganyiko ulipotokea kuhusu wagonjwa wawili waliokuwa hawajitambui.

Mmoja kati yao ndiye alihitaji upasuaji wa kichwa ili kuondoa damu iliyokuwa imeganda kwenye ubongo wake.

Huyo mwingine alikuwa amefurwa kwenye kichwa lakini alihitaji matibabu ambayo hayakushirikisha upasuaji.

Lakini asiyehitaji upasuaji ndiye aliyeishia kufanyiwa upasuaji. Madaktari waligundua kosa hilo saa chache baada yao kuanza upasuaji walipogundua kwamba hawakuweza kuiona damu iliyoganda kwenye ubongo wa mgonjwa waliokuwa wanamfanyia upasuaji.

Bi Koros ameomba radhi na kusema "tunafurahi kuwatangazia umma kwamba mgonjwa huyo sasa ametibiwa na anaenedelea vizuri kupata nafuu".
Hili sio sakata la kwanza kukumba hospitali hiyo, mwezi wa kwanza mwaka huu, waziri wa afya nchini Kenya Dkt Cleopha Mailu aliamrisha uchunguzi ufanyike baada ya wanawake waliojifungua kudai kwamba wanadhalilishwa kingono.

Taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao zilidai kina mama waliojifungua wamekuwa wanashambuliwa na baadhi ya wafanyikazi wakati wakienda kwenye chumba cha watoto wachanga kuwanyonyesha watoto wao.

Tukio hilo liliibua maandamano na wanaharakati na wanawake walikasirishwa na usalama duni na utendaji kazi wa hospitali hiyo.

Kisa karibu sawa Tanzania

Kwa upande wa Tanzania, kisa kama hiki kiliwahi kutokea mwaka 2007.

Tarehe 8 Novemba, madaktari wawili wa upasuaji wa ubongo katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili walimpasua kichwa Emmanuel Didas kutoa uvimbe ambao haukuwepo.

Wakati mgonjwa Emmanuel Mgaya, aliyekuwa na uvimbe huo alipasuliwa goti.

Madaktari hao walichukuliwa hatua na kufutwa kazi na mamlaka ya hospitali.

Makosa Uingereza na India

Si Afrika pekee ambapo makosa kama hayo hufanyika. Kipindi cha BBC cha Victoria Derbyshire mwaka jana kilibaini kwamba makosa takriban 1,400 hufanyika kila wiki katika hospitali za kujifungulia kina mama nchini England kila wiki.

Mwishoni mwa mwaka jana nchini India, mtoto aliyekuwa amedaiwa kufariki baada ya kuzaliwa katika hospitali moja mji mkuu wa Delhi alibainika kuwa hai jamaa zake walipokuwa wanaelekea kumzika.

Alhamisi, 1 Machi 2018

Mwanamuziki Ney wa Mitego asema yeye ndio chanzo cha nyimbo kufungiwa Tanzania


Mwanamuziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki, alimaarufu kama Ney wa Mitego amesema yeye ndio chanzo cha maamuzi ya nyimbo kufungiwa Tanzania.

Nyimbo zaidi ya kumi zilitangazwa na Mamlaka ya Mawasiliano kupigwa marufuku kuchezwa katika radio nchini Tanzania.

'Wakati mwingine naona kuwa sababu ya kufungiwa kwa miziki hii ni mimi na wengine wanawekwa kama chambo kwa kuwa kati ya nyimbo zote hizo,nyimbo mpya peke yake ni yangu tu ambayo imetoka wiki mbili zilizopita na video ina wiki moja tu" Ney wa Mitego.

Hata hivyo hii sio mara ya kwanza kwa mwanamuziki huyo kupata misukosuko katika muziki wake.

Mnamo mwezi machi mwaka jana Ney wa Mitego aliwahi kukamatwa na jeshi la polisi la Tanzania kwa kosa la kuimba wimbo unaokashifu serikali lakini inakumbukwa kuwa mwanamuziki huyo aliwahi kupewa onyo kuhusiana na mavazi yake.

Huku wanamuziki wengine bado hawakuwa tayari kutoa maoni yao.

Wakati huo huo , hii leo, msanii wa bongo fleva, Roma Mkatoliki aliyefungiwa wimbo wake mpya wa 'kibamia' kwa sasa amefungiwa na Naibu Waziri wa habari,sanaa,utamaduni na michezo Juliana Shonza kutojihusisha na tasnia ya muziki kwa takribani miezi sita mara baada ya kukiuka kurekebisha wimbo huo .

Baadhi ya wananchi walioongea na BBC,walikuwa na maoni tofauti.


Meneja wa mawasiliano wa TCRA,Semu Mwakyanjala amelizungumzia suala la muda na kusema kuwa 'wakati wa kufungia haujalishi kikubwa ni nyimbo hizo zilizofungiwa ni hazina maadili.'

Muasi wa zamani ageuka kuwa mlezi wa yatima Burundi

Mwanamke mmoja nchini Burundi ambaye alikuwa ni miongoni mwa wanawake wa kwanza kujiunga na makundi ya waasi mwishoni mwa miaka ya 90, kwa sasa amejiingiza katika shughuli za kuwalea watoto yatima.
 Bi Mariam Ndayisenga maarufu kama Mama Zulu,muasi mstaafu aliyeamua kuwalea watoto yatima

Athari za vita kwa watoto ndio zilizomuhamasisha mwanamke huyu ambaye alikuwa mpiganaji wa zamani wa kundi la Waasi la CNDD/FDD kufanya kazi ya kuwalea watoto hao yatima.

Kituo chake kina watoto zaidi ya 70 wenye rika mbalimbali wakiwemo hata watoto wachanga.


Kituo hiki kinaonekana kuwa sio cha kawaida kutokana na historia ya mmiliki wa kituo hicho kuwa mstaafu katika harakati za kijeshi.

Lakini ni nini kilichomsukuma kuanza kushughulika na kazi ya kulea yatima na kuacha shughuli za uasi.

''Mimi ni mama wa kwanza kabisa kuchukua silaha na kwenda kupigania nchi yangu lakini matokeo yake sikuwa ninayategemea kwa kuwa yalileta athari kubwa sana haswa kwa watoto.'' Bi Marium aeleza.

Katika vita alikutana na changamoto mbalimbali lakini kulea watoto hawa inampa furaha kwake na anasema hudumu za watoto kuanzia chakula , mavazi hata matibabu imekuwa sio jambo rahisi, lakini hajavunjika moyo na watu pia wanamsaidia kwa namna moja au nyingine.

Pamoja na kukutana na changamoto kadha wa kadha hata kwenye malezi ya watoto wahitaji Maryam anasema katika maisha yake amezoea kupambana.

Maana hata wakati wa vita alipewa jina la mama Zulu kwa kuwa yeye ni mama shujaa na hata anadhani ushujaa wake unahitajika kuwalea watoto hawa zaidi.

Burundi ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizokumbwa na vita na kujikuta watoto wengi wako barabarani wakiwa ni omba omba na mayatima.

Hivyo changamoto kubwa iliosalia ni jinsi ya kuwatunza watoto hao wahitaji na yatima nchini humo.

TAMBUA KANUNI ZA KUISHI NA WATU VIZURI

Mojawapo ya mambo muhimu katika mafanikio ya aina yoyote maishani ni kupata msaada wa aina Fulani kutoka kwa watu wengine. Mtu hawezi kufan...